Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amesema kuwa amechukua fomu ya kugombea urais kwa awamu ya pili ili amalizie kazi iliyobaki katika kuijenga Tanzania ya viwanda.

Akizungumza hivi karibuni na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho jijini Dodoma, muda mfupi baada ya kuchukua fomu, Rais Magufuli amesema kuwa kuijenga Tanzania ya Viwanda kunaendana na kuhakikisha kuna umeme wa kutosha.

Hivyo, Serikali inakamilisha mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme (Julius Nyerere Hydropower Station) ambalo litakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawatt 2115. Kukamilika kwa mradi huo kutasaidia uwepo wa umeme wa kutosha kuwezesha viwanda na kupunguza gharama ya umeme kwa wananchi.

Rais Magufuli alisema kuwa viwanda hivyo vitasaidia kukamilisha uzalishaji wa bidhaa kama nguo, na kuachana na utamaduni wa kuvaa mitumba inayoagizwa kutoka nje. Amesema anataka Tanzania iwe inaziuzia nguo nchi za Ulaya, ikiwezekana iwe ni mitumba.

“Pamba inalimwa kwetu, inasafirishwa nje, inaenda kuongezewa thamani kwa kutengenezewa nguo, wanazivaa kisha wanatuletea sisi kama mitumba. Nataka tutoke huko, pamba zetu zipelekwe kiwandani, ziongezewe thamani, nguo zishonwe,ikiwezekna tuvae kwanza ndio tuwapelekee Ulaya,” amesema.

Tangu aingie madarakani, wananchi wengi wameunganishiwa umeme, hususan sehemu za vijijini.

“Sasa hivi vijiji 9400 vina umeme bado vijiji 3,000, najua tutabana wapi, na tutabana mafisadi gani watapike hela ili tupeleke kwenye mradi wa kufua umeme,” amesema Rais Magufuli.

Watoto wafariki wakiwa wamelala, mama aliwasha jiko la mkaa kupata joto

Waziri Mpango: PPRA wanafanya kazi nzuri, waongeze elimu kwa umma

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 10, 2020
Waliokuwa Makomando wa Marekani watupwa jela kwa kujaribu kumteka Rais