Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tano, John Pombe Magufuli amesema kwa sasa hatoweza kusafiri kwenda nchi yeyote, ataendelea kumtumia muwakilishi wake ili yeye abaki kuinyoosha nchi na kuwashughulikia Watanzania wajanja.
Amesema hadi sasa amepata mialiko 60 kutoka nchi za nje mbalimbali, lakini hatokwenda.
Ameeleza kuwa alitakiwa kusafiri kwenda Ethiopia kwenye Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU), lakini ameona amtume Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ili amuwakilishe ili yeye aendelee na majukumu mengine ya nchi.
Magufuli amewaomba Watanzania wenye nia njema na nchi yao wamuombee ili ashughulikie changamoto za nchi hii kwani anawasiwasi anaweza kumaliza kipindi chake cha uongozi na mambo yakabaki hivyohivyo.
”Ndiyo maana sitembei sana, nimeshapata mialiko 60, siendi, nikienda huko watafanya ajabu ngoja nideal nao kwanza’ amesema Magufuli.
Magufuli alitoa kauli hizo jana mjini Sengerema katika ziara yake ya uzinduzi wa mradi wa maji wa Nyamazugo, mkoani Mwanza.