Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameeleza kutoridhishwa na usimamizi wa Wizara ya ujenzi uliopelekea uharibifu wa barabara ya kilometa 90 inayotumiwa na wananchi kutoka Mtwara na Lindi kwenda Dar es salaam.
Amebainisha hayo leo Julai 30, 2020 aliposimama Nangurukuru kuongea na wananchi akiwa njiani kuelekea Dar es salaam baada ya kuongoza taifa kwenye mazishi ya Rais wa awamu ya tatu hayati Benjamin Mkapa yaliyofanyika jana.
“Hii barabara imeharibika, huwezi ukaamini kama tuna Waziri wa Ujenzi, Naibu waziri wa Ujenzi au Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, au ‘Cheif Excutive’ Amesema Rais Magufuli.
Amebainisha kuwa uzembe mkubwa walioufanya ni kwa kuruhusu magari mazito yanayobeba ‘jipsum’ kupita kwenye barabara hiyo nakufanya uharibifu mkubwa.
Rais Magufuli amesema barabara hiyo haina hali sawa na ile aliyoiacha wakati akiwa waziri wa ujenzi na kuiambia wizara hiyo ijipange vizuri kutatua tatizo la ubovu wake.
Aidha amewapa pole wananchi wanaotegemea barabara hiyo na kuwaahidi ataifanyia kazi punde atakapo rejea Ikulu.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Barabara, Barabara ikishakua ya lami inapata 100% ya ukarabati , Fedha za Bodi ya Mfuko wa Barabara sijui zinakwenda wapi, Serikali haijalala, hili la ubovu wa Barabara nawahakikishia nitalishughulikia mwenyewe” Amesema Rais Magufuli.