Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Chile Juan Antonio Pizzi amempongeza Claudio Bravo kwa kazi nzuri aliyoifanya usiku wa kuamkia leo, katika mchezo wa nusu fainali wa kombe la mabara dhidi ya mabingwa wa soka barani Ulaya Ureno.
Bravo alipangua mikwaju mitatu ya penati na kuiwezesha Chile kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa mikwaju mitatu kwa sifuri.
Pizzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Bravo alikua shujaa katika mchezo huo na hana budi kutoa pongezi zake za dhati kwa kazi nzuri aliyoifanya.
Alisema mbali na ushujaa wa kupangua mikwaju mtitatu ya penati, mlinda mlango huyo wa klabu ya Man City alifanya kazi nzuri katika kipindi chote cha dakika 120 ambacho kilishuhudia timu hizo zikishindwa kufungana.
Bravo alipanguwa mikwaju ya penati iliyopigwa na Ricardo Quaresma, Joao Moutinho na Nani huku mikwaju ya Chile iliyokwamishwa wavuni ikipigwa na Vidal, Charles Aranguiz na Alexis Sanchez.
“Ninafuraha isiyo kifani, lakini yote haya yamesababishwa na mlinda mlango wangu Bravo kwa kazi nzuri aliyoifanya, nitampongeza bila kuchoka maana ametuwezesha kushangilia kwa furaha.” Alisema Pizzi
“Tulishindwa kufunga katika muda wa kawaida, lakini hilo halikuwazuia wapinzani wetu kutafuta namna ya kutushinda ndani ya muda wa dakika 120, ila umahiri wa Bravo ulisitisha mipango yote ya Ureno.”
Chile watacheza mchezo wa fainali mwishoni mwa juma hili dhidi ya mshindi wa mchezo wa nusu fainali ya pili utakaochezwa leo, kati ya mabingwa wa soka wa dunia timu ya taifa ya Ujerumani dhidi ya mabingwa wa Amerika ya kati na kaskazini Mexico.