Kiungo wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC Juan Cuadrado, amesema katu hawatorejea makosa waliyoyafanya wakati wa mchezo dhidi ya Man Utd, ambao ulishuhudiwa wakipoteza nyumbani kwa kufungwa mabao mawili kwa moja, majuma matatu yaliyopita.
Cuadrado ametoa msisitizo huo, wakati kikosi chao kikiwa kwenye mtihani wa kuikabili Valencia ya Hispania leo usiku, kwenye uwanja wa Mestella.
Kiungo huyo amesema hatua ya kufungwa na Man Utd, imewafunza mambo mengi, ambayo wameshayafanyia kazi katika maandalizi yao kuelekea mchezo dhidi ya Valencia, ambao watahitaji kushinda ili kujihakiishia kufuzu hatua ya 16 bora ya ligi ya mbingwa brani Ulaya msimu huu.
Mbali na ushindi, matokeo ya sare ya aina yoyote pia yataibeba klabu hiyo ya mjini Turin na kutinga kwenye hatua ya 16 bora.
“Tulifanya makosa makubwa sana katika mchezo wetu dhidi ya Man Utd, hatukupaswa kufungwa, lakini hali hiyo ilitokea na kutusababishiwa kushindwa kufikia lengo la kusonga mbele kwenye hatua ya 16 bora, hatutaki jambo hilo lijirudia katika mchezo unaotukabili dhidi ya Valencia, tutalazimika kupambana ili turekebishe makosa yetu.”
“Ninaamini matokeo mazuri yatapatikana, tupo tayari kwa lolote kwenye mchezo huu, lengo hapa ni kuhakikisha tunavuka na kwenda kwenye hatua nyingine.” Alisema kiungo huyo kutoka nchini Colombia.
Hata hivyo katika mchezo dhidi ya Valencia, Juventus FC watamkosa kiungo mshambuliaji Federico Bernardeschi, ambaye anakabiliwa na majeraha ya misuli.
Wakati huo huo kikosi cha Velencia, kitahitaji ushindi katika mchezo wa leo dhidi ya Juventus ili kujiweka kwenye mzingira mazuri ya kuwania nafasi ya kutinga kwenye hatua ya 16 bora.
Ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Young Boys walioupata majuma matatu yaliyopita, umekua chachu kwa kikosi cha Marcelino kuwa na ari ya kuapambana hii leo, ili kutimiza lengo la kubaki kwenye michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu.
Jambo lingine linalowapa ujasiri Valencia, ni ushindi wa michezo miwili mfululizo ya ligi ya Hispania dhidi ya Getafe na Rayo Vallecano.
Meneja Marcelino García Toral amewaambia waandishi wa habari kuwa: “Utakua mchezo mgumu, lakini kikosi changu kinajua nini cha kufanya ili kufanikisha lengo la kushinda kwenye uwanja wa nyumbani.”
“Katika mchezo wa soka, jambo la kwanza ni kuhakikisha unapambana ili upate matokeo mazuri, ukishindwa hilo unalazimika kupigania hata sare na mambo yakiwa magumu zaidi huna budi kupoteza mchezo.” Aliongeza meneja Marcelino.
“Juventus wameshadhihirisha ni klabu ya aina gani barani Ulaya, lakini hilo halitupi wasiwasi, zaidi ya kuendelea kujiamini ili kufanikisha mipango yetu kuelekea mchezo wa kesho (Leo).”
Kwenye mchezo wa kwanza uliozikutanisha klabu hizo, Juventus walifanikiwa kuifunga Valencia mabao mawili kwa sifuri.
Mabingwa wa soka nchini italia Juventus wanaongoza msimamo wa kundi -H wakiwa na alama tisa, wakifuatiwa na Manchester United wenye alama saba, Valencia wanashika nafasu ya tatu kwa kumiliki alama tano na Young Boys wanaburuza mkia kwa kuwa na alama moja.