Kiungo kutoka nchini England Jude Bellingham anakuwa mchezaji wa nne wa Real Madrid kufunga mabao katika mechi ya kwanza ya La Liga na Ligi Mabingwa Ulaya baada ya kusajiliwa akimfikia Cristiano Ronaldo.
Bao la Bellingham dhidi ya Union Berlin dakika ya 94 liliipa ushindi wa bao 1-0 Madrid kwenye mechi yao ya ufunguzi wa Ligi Mabingwa Barani Ulaya juzi Jumatano (Septemba 20).
Alifunga pia bao lake la kwanza La Liga dhidi ya Athletic Club, na tangu hapo alifunga mabao mawili mengine dhidi ya Almeria kabla ya kufunga tena dhidi ya Celta Vigo na Getafe.
Sasa Kiungo huyo amefuata nyayo za Ronaldo, Isco na Marco Asensio ambao waliwahi kufanya hivyo.
Bila shaka Ronaldo ambaye anakipiga Al-Nassr kwa sasa alikuwa na mafanikio mengi Los Blancos kabla ya kuondoka sambamba na Isco na Asensio, ambao wametimka pia.
Isco anakipiga Real Betis kwa sasa huku Asensio alijiunga na Paris Saint Germain kwenye usajili wa dirisha la kiangazi lililopita.
Bellingham amefunga mabao sita katika mechi sita za mwisho alizocheza. Na alipokuwa Borussia Dortmund alifunga mabao manne katika mechi 132 alizocheza.
Pia alifunga mabao manne katika mechi 44 Birmingham. Kiungo huyo pia amefunga mabao mawili kwa taifa lake.