Kocha Mkuu wa Real Madrid Carlo Ancelotti amekiri kushangazwa na jinsi Jude Bellingham anavyoendelea kupachika mabao baada ya kiungo huyo wa kati wa Real Madrid kufunga mabao mawili katika ushindi wa 2-1 wa El Clasico dhidi ya FC Barcelona juzi Jumamosi (Oktoba 28), akisema kwamba kwa sasa kiungo huyo ndiye mchezaji anayeleta mabadiliko.
Bellingham aliisawazishia Real Madrid dakika ya 68 kwenye Uwanja wa Olympic baada ya lkay Gündogan kuiweka Barca mbele dakika ya sita kabla ya kufunga bao la ushindi katika muda ulioongezwa na kuwaacha Madrid kileleni mwa msimamo wa La Liga kwa alama 28.
“Alifunga bao la ajabu la kwanza na alikuwa mwerevu kwa la pili,” alisema Ancelotti katika mkutano wake na wana- habari baada ya mechi.
“Tunashangaa. Kila mtu anashangazwa na kiwango chake, na kiwango chake cha ufanisi pale mbele.
“Anaingia kwenye eneo la hatari, lakini juzi shuti la bao la kwanza lilitushangaza, alifunga bao zuri sana… Hivi sasa yeye ndiye mchezaji anayeleta mabadiliko.”
Nyota huyo wa England sasa ana mabao 10 katika mechi 10 za ligi msimu huu na kumfanya kuwa mfungaji bora kwa sasa na 13 katika mashindano yote baada ya kufunga matatu kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.
“Anaonekana kama mkongwe, mtazamo wake ni mzuri sana,” Ancelotti alisema.
“Bao la kusawazisha lilibadilisha nguvu kabisa, lilimaanisha nguvu zaidi kwetu na udhaifu zaidi kwa FC Barcelona, ambao walikuwa wamecheza vizuri hadi wakati huo.” Mshirika wa Bellingham katika nafasi ya kiungo, Luka Modric aliongeza sifa kwake.