Kocha Mkuu wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amemmwagia sifa kiungo wake kutoka nchini England Jude Bellingham baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Getafe.
Bellingham alifunga bao la ushindi dhidi ya Getafe katika dakika ya 90 na kuipa Real ushindi wa mabao 2-1 juzi huku kocha wake akipagawa na kiwango staa huyo.
Baada ya mchezo huo kumalizika Ancelotti alisema: “Sikushangazwa na ubora wake hata kidogo, Kinachonishangaza amefunga mabao mengi katika mechi chache, kila mtu ameshangazwa na kasi ya Bellingham, ni mchezaji mzuri na ameonyesha kwamba hataki masihara hata kidogo,”
Kiungo huyo amekuwa gumzo Santiago tangu aliposajiliwa akitokea Borussia Dortmund kwa ada ya uhamisho wa Pauni 88.5 milioni kwani tayari ameanza kutengeneza jina lake Hispania ambako katika mechi nne za Laliga amefunga mabao matano.
“Kikosi kinatakiwa kucheza kwa kiwango cha hali juu mfano mzuri Bellingham. Amezoea mazingira haraka sana, alikuwa mapumziko na wachezaji wenzake hivi karibuni nadhani ni jambo zuri, anaweza kufunga mabao 15 kwa sababu aliwahi kufunga alipokuwa Dortmund.
“Anakaa na mipira na hapotezi krahisi. Mara nyingi anapenda kuingia eneo la hatari ndio maana anafunga mabao mengi,” aliongeza Anelotti.
Bellingham amejumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya England kwa ajili ya mechi ya kufuzu Kombe la Mataifa Ulaya (EURO 2024).