Jukwaa la wahariri nchini leo limepinga rasmi uamuzi wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye kulifuta Gazeti la Mawio.

Akiongea na waandishi wa habari, Katibu wa Jukwaa la Wahariri, Neville Meena amesema kuwa taratibu zilizotumika kulifungia gazeti hilo ni kinyume na misingi ya utawala bora.

Alisema kuwa mfumo unaotumika hivi sasa kutatua migogoro katika tasnia ya uandishi wa habari ni kandamizi kwa kuwa inampa nguvu kubwa Waziri ambapo anakuwa Mhariri Mkuu.

“Mfumo wa sasa wa kushughulikia kasoro za kitaaluma katika vyombo vya habari ni kandamizi. Kwanza inamfanya waziri kuwa Mhariri Mkuu na ana mamlaka ya kutoa adhabu kwa kuzingatia mtazamo wake, hata kama mtazamo huo unakinzana na misingi ya kitaaluma,” alisema Meena.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa hilo la Wahariri, Absalome Kibanda alieleza kuwa hakukuwa na ulazima wa kulifuta gazeti hilo kama alivyofanya waziri mwenye dhamana kisheria.

Kibanda alisema kuwa hata katika nchi nyingine serikali huwa katika migogoro na baadhi ya magazeti na kutokubaliana na mienendo yake lakini huwa hawachukui uamuzi wa kuyafuta kwani kufanya hivyo ni kuziba uhuru wa vyombo vya habari.

Mwenyekiti huyo wa Jukwaa la wahariri alionesha wasiwasi wake kama wahariri watamuunga mkono Waziri Nape katika kuandaa muswada wa sheria mpya ya vyombo vya habari kutokana na kile alichokifanya.

 

Maafande Watuma Salamu Kwa Ndugu Zao Wa Mbeya
Simba Waendeleza Ushindi Ligi Kuu Tanzania Bara