Vijana Wazalendo wametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua alizozichukua kuwapinga wanyonyaji wa uchumi na raslimali za nchi kupitia sekta ya Nishati na Madini.
Pongezi hizo zimetolewa mapema hii leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wazalendo Tanzania, Mwita Nyarukururu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema kuwa ana hakika watanzania wanafuatilia juhudi za Rais Magufuli katika sekta ya Nishati na Madini kwa kuunda Tume ya wataalam mbalimbali kufanya uchunguzi na upembuzi yakinifu katika madini mchanga wa Madini.
“Wote tumeshuhudia ripoti ya wataalam wa madini chini ya Mwenyekiti, Prof. Abdulkadir Mruma ambapo Tume imeeleza masikitiko yake makubwa dhidi ya makampuni ya madini nchini yanavyokwapua na kusafirisha rasilimali zetu bila Taifa kunufaika”, amesema Mwita