Nyota wa zamani wa Timu ya taifa ya Brazil na klabu za Barcelona na Chelsea Juliano Haus Belletti amewatia moyo wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ambao keshokutwa Jumamosi (Juni 04) wataanza Kampeni ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za AFCON 2023, kwa kucheza dhidi ya Niger nchini Benin.
Belletti alitumia wasaa wa safari yake nchini Tanzania kwa ajili ya ziara ya Kombe la FIFA la Dunia kukutana na wachezaji wa Taifa Stars ambao leo Alkhamis (Juni 02) wameanza safari ya kuelekea nchini Benin.
Gwiji huyo ambaye alikua akicheza nafasi ya Beki wa Kulia, alitembelea mazoezi ya mwisho ya Taifa Stars jana Jumatano (Juni Mosi), Uwanja wa Benjamin Mkapa na kupata fursa ya kuzungumza na wachezaji wote.
Belletti aliwaambia wachezaji wa Stars, wanapaswa kupambana kwa malengo, huku akiwasisitiza umoja na mshikamano wakati wote watakapokua kwenye uwanja wa mapambano kwa ajili ya Taifa lao.
Alisema katika soka hakuna kinachoshindikana, kwani hata timu ya taifa ya Brazil ilivyotwaa Ubingwa wa Dunia mwaka 2002 Korea Kusini na Japan, ilijengwa na vitu hivyo ambavyo ni silaha kubwa michezoni.
“Wakati tukiwa nchini Japan na Korea Kusini mwaka 2002, Brazil haikuwa sehemu ya timu zilizopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Dunia, watu walizungumzia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, lakini hawakufikiria namna tulivyokua tumejiandaa kwa ajili ya michuano ile.”
“Ndani yetu kama timu tulikua na siri kubwa ya umoja na mshikamano na kila tulipokwenda Uwanjani tulihimizana hilo, na ndio maana tulifanikiwa kuvuka hatua ngumu na kufika fainali na kutwaa ubingwa wa Dunia.”
“Mnatakiwa kuwa na hivyo vitu, kwa sababu mkiaminiana katika umoja na mshikamano, hakuna kitakachoshindikana kwenye kampeni yenu ya kucheza Fainali za Afrika, ninawakia kila la kheri.” Alisema Belletti.
Belletti alikua sehemu ya maafisa wa FIFA waliotua nchini Tanzania juzi Jumanne (Mei 31), kwa ajili ya kulitembeza Kombe la FIFA la Dunia nchini humo.