Baada ya kufanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii 2023 kwa kuifunga Young Africans iliyokuwa bingwa mtetezi, Uongozi wa Klabu ya Simba SC umepewa ushauri wa bure kwa kutakiwa kulipa muda Benchi la ufundi la na mastaa wao katika hatakari za Mshike Mshike wa msimu mpya wa 2023-24.
Angalizo hilo kwa mabosi wa Simba SC limetolewa na kocha wao wa zamani, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye alikuwa shuhuda wa michezo yote ya Wekundu wa Msimbazi iliyochezwa jijini Tanga juma lililopita, huku wakishinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati dhidi ya Singida FG na kisha Young Africans.
Kocha huyo mzawa amesema suala la ushindi wa mikwaju wa Penati ni la kawaida katika mchezo wa soka, lakini kinachotakiwa ni kuhakikisha Kocha na Benchi lake la Ufundi pamoja na wachezaji kwa ujumla wanapewa nafasi ya kutosha ili kuweza kujenga kikosi imara kwa ajili ya mshike mshike wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.
Julio amesema usajili wa wachezaji na kuonyesha uwezo uwanjani ni vitu viwili tofauti, hivyo ni lazima Uongozi, Mashabiki na Wanachama wawe wavumilivu kwa sasa ili kuwapa muda mastaa wao wazoeane na kisha wawapime mbele ya safari.
“Niliitazama Simba katika mchezo wa Simba Day na michezo miwili waliocheza jijini Tanga (nikimaanisha dhidi ya Singida FG kisha Young Africans), kuna matatizo madogo yanayorekebishika ila viongozi wawape muda wa kutosha benchi la ufundi na wachezaji katika kuweka mambo sawa,” amesemna Julio.
Julio amesema hata misimu minne mfululizo Simba ilivyokuwa haishishiki ndani na hata nje ilikuwa na kikosi bora ambacho kilikaa na kutengenezwa kwa muda mrefu, hivyo wanasimba wasiharakishe mambo, kwani wakifanya hivyo watawachanganya wachezaji na makocha.
“Walikuwepo kina Luis Miquissone walipoondoka sambamba na Clatous Chama mambo yakaanza kuyumba walipokuja wengine walishindwa kuingia katika mfumo haraka ndio mpira ulivyo,” alisema Julio
Tayari kikois cha Simba Sc kimeshawasili mkoani Morogoro kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu 2023/24 dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa keshokutwa Alhamis (Agosti 17) katika Uwanja wa Manungu Complex, uliopo wilayani Mvomero.