Aliyewahi kuwa Kocha na Mchezaji wa Simba SC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ameibuka na kutamka kuwa, Young Africans ni bora kwa sasa kutokana kiwango bora ambacho wanachokionyesha.
Kauli hiyo imekuja hivi sasa baada ya timu hiyo, kutoka kupata ushindi mnono katika Ligi Kuu Bara ikitoka kuwafunga KMC FC na JKT Tanzania kwa mabao 5-0 kila moja na Namungo 1-0.
Young Afrocans pia imetoka kuwafunga Al Merreikh ya nchini Sudan mabao 2-0 ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Kigali Pele huko nchini Rwanda ambako timu hiyo inautumia kama uwanja wao wa nyumbani.
Katika msimu huu, Young Africans imeonekana kuanza vema huku ikisifiwa na baadhi ya makocha kutokana na ubora wao wanaouonyesha.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Julio amesifu ubora wa kikosi cha Young Africans katika msimu huu kutokana na kiwango wanachoendelea kukionyesha katika Michezo ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Julio amesema kuwa, ubora huo wa Young Africans umetokana na kukaa pamoja muda mrefu huku wakiingiza maingizo machache ya wachezaji katika msimu huu ambao wameongeza chachu ya ushindi.
“Young Africans wanacheza vizuri kwa sababu wamekaa pamoja muda mrefu na wameingiza watu wachache ambao wamekuja kuleta chachu timu ifanye vizuri katika msimu huu.”
“Kikubwa mashabiki wa Young Africans, wanatakiwa kumpa muda zaidi kocha kuandaa timu yake, ninaamini watafanya vizuri zaidi katika msimu huu.
“Napongeza usajili mkubwa ambao wameufanya katika msimu huu, ambao umeleta hali ya kila mchezaji kupambania namba,” amesema Julio.