Beki mkongwe wa pembeni nchini, Juma Abdul wa Singida Fountain Gate yupo mbioni kutua Namungo kwa mkopo baada ya kukosa namba ndani ya kikosi hicho msimu uliopita.

Abdul, aliyewahi kuwika na Mtibwa Sugar, Young Africans na Taifa Stars ni miongoni mwa mabeki wazawa wenye uwezo mkubwa uwanjani, lakini hakuwa na msimu mzuri ndani ya Singida iliyomaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara iliyocheza kwa msimu wa kwanza na kukata tiketi ya michuano ya CAF, ataungana na wenzake wengine wenye mikataba kutolewa kwa mkopo katika timu nyingine.

“Juma Abdul bado ana mkataba alisaini miaka miwili, lakini kutokana na kukosa namba ndani ya timu inamuacha akajaribu maisha kwingine,” alisema mtoa habari hizi.

Rafiki wa beki huyo amesema Abdul aliamua kuichagua Namungo FC ili kuitumikia katika msimu ujao 2023/24.

Hata hivyo alipotafutwa Abdul kuzungumzia hatima yake ndani ya Singida alisema: “Miye bado ni mchezaji wa Singida kama ikitokea lolote basi uongozi utasema,”alisema Abdul

Naye Msemaji wa Singida Hussein Massanza alipoulizwa, amesema wataweka hadharani kila kitu kuhusu usajili wao kabla ya wikiendi hii wakati timu ikienda Arusha kuweka kambi ya maandalizi ya msimu.

Maonyesho ya sabasaba kufungwa leo
Wanafunzi waathirika wakuu Dawa za Kulevya - Kamishna DCEA