Aliyekua beki na nahodha msaidizi wa Young Africans, Juma Abdul amesema kwa sasa anafikiria zaidi kucheza soka la kulipwa na kuna dili analisubiri na kama likitiki ataondoka nchini.

Beki huyo anaesifika kwa mipira ya Krosi amesema kwa sasa hajasaini timu yoyote hapa nchini, labda dili lake la kwenda nje likikwama ndipo anaweza kufikiria timu nyingine ya kujiunga nayo katika kipindi hiki kifupi kilichosalia kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili mwishoni mwa mwezi huu.

Juma amesema endapo dili la kwenda nje nchi halitafanikiwa kwa sasa anaweza kusaini timu yoyote ya Ligi Kuu kwa mkataba usiozidi miezi sita.

“Hata kama hilo dili la nje halitafanikiwa kwa sasa, naweza kusaini timu yoyoye kwa miezi sita tu wakati naendelea kufanya mipango mingine ya kucheza nje ya nchi” amesema Juma.

Moja ya timu inayomuhitaji mchezaji huyo hapa nchini ni Namungo FC ambayo itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao.

Juma pamoja na beki mwenzake Kelvin Yondani walitangazwa kuachwa na klabu ya Young Africans, ambayo waliitumikia kwa miaka minane.

Inadaiwa kuwa uongozi wa klabu ya Young Africans iliachana na wachezaji hao wawili kwa madai ya kushindwana katika maslahi.

Hata hivyo ndani ya siku mbili hizi kumeibuka maneno kuwa klabu hiyo huenda ikawaita mezani wachezaji hao wazoefu ili kufanya nao mazungumzo ya kuwemo katika kikosi kitakachopambania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Lakini taarifa hizo zimekanushwa na Juma Abdul, kwa kusema, hafahamu lolote zaidi ya kuangalia mambo yake ya kuhakikisha anapata timu ya kuitumikia nje ya nchi.

“Sijapata hizo taarifa zaidi ya kusikia kama wewe, na sidhani kama zina ukweli”

Alipoulizwa kama ni kweli je yupo tayari kurudi Young Africans, amesema, “Siwezi kujibu hilo, ni ngumu kutoa jibu la moja kwa moja wakati huu”

“Ujue kwa sasa nafikiria zaidi kwenda nje ya nchi kwa sababu kuna dili nalisubiria na kama likienda vizuri naenda kucheza huko”

“Siwezi kusema nani ananifanyia dili hilo wala timu gani inanihitaji ila ndani ya siku tatu hivi nitajua mustakabali na uelekeo wangu wa wapi nitaenda” amesema Juma

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa kampuni ya GSM ambao ni wadhamini wa Young Afrucans ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo Hersi Said alipoulizwa kuhusu tetesi za kuwarejesha wachezaji hao, alijibu kwa ufupi “Hakuna kitu kama hicho”

Wachezaji wengine walioachwa Young Africans katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni pamoja na Mrisho Ngasa, David Molinga, Jaffary Mohamed, Tariq Seif, Andrew Vicent, Papy Tshishimbi na Mohamed Issa.

Wengine ni Ally Mtoni, Muharami Issa, Yikpe, Ali Ali, Patrick Sibomana, Eric Kabamba na Raphael Daud.

Idara za serikali chapeni kazi zenu TSN
TCU yafungua dirisha 2020/21