Kiungo mshambuliaji wa mabingwa wa soka Tanzania bara Young Africans, Juma Mahadhi, amesema yu radhi kuachwa na klabu hiyo, ili kuepuka mpango wa kupelekwa kwa mkopo katika klabu nyingine.

Mahadhi alitua Young Africans msimu uliopita akitokea Coastal Union ya jijini Tanga, na katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kiungo huyo alionyesha kiwango cha juu.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Young Africans wana mpango wa kumpeleka Mahadhi kwa mkopo katika klabu ya Singida United inayonolewa na Mholanzi Hans van der Pluijm.

Mahadhi amesema, tayari ameshapata ofa kutoka katika klabu za ndani na nje ya nchi, lakini anaheshimu mkataba wake wa mwaka mmoja uliobakia ndani ya Young Africans.

“Sipo tayari kutolewa kwa mkopo, nina ofa za ndani na nje ya nchi lakini nasubiri kujua hatma yangu ndani ya Young Africans, ni bora waniache nikatafute riziki mahali pengine nitakaporidhia mwenyewe, uwezo bado ninao,” Alisema Mahadhi.

Mshambuliaji huyo aliongeza kuwa, anaamini atakapokutana na viongozi wake watazungumza na kufikia muafaka kuhusiana na suala hilo kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.

Gambo azidi kuing'arisha Arusha, ateta na wawekezaji
Nyumbani Ni Nyumbani - Klaas-Jan Huntelaar Atua Amsterdam Arena