Kaimu Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba Juma Mgunda amesema ana kazi kubwa kuhakikisha kikosi chake kinafanya vizuri katika Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Simba SC ilikata Tiketi ya kutinga Hatua ya Makundi kwa kuifunga CD Primeiro De Agosto ya Angola kwa ushindi wa jumla wa 4-1, baada ya kucheza nyumbani na ugenini.
Mgunda amesema hana budi kuwa tayari kwa michezo ya hatua ya Makundi, kwani anafahamu Hatua hiyo ni ngumu zaidi kuliko hatua ya awali ambayo amefaulu kwa asilimia 100.
“Ninashukuru Mungu Malengo tuliojiwekea ya kuingia Hatua ya Makundi tumefanikiwa, sasa kazi iliyopo mbele yangu ni moja ya kukiandaa kikosi ipasavyo ili kiweze kufanya vizuri kwa Hatua tulioingia ambayo ni ngumu zaidi.”
“Kazi niliyonayo ni nzito, Programu ya mazoezi itakua ngumu sana na wachezaji wanalijua hilo na wakati ukifika nitauzungumzia zaidi kuhusu maandalizi yetu Kimataifa.” amesema Kocha Mgunda
Baada ya kufuzu Hatua ya Makundi Ligi ya MaBingwa Barani Afrika Simba SC imeungana na klabu za Al Ahly (Misri), Wydad AC (Morocco), Espérance de Tunis (Tunisia), Raja Casablanca (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini).
Nyingine ni Zamalek (Misri), Petro de Luanda (Angola), Guinea Horoya (Guinea), CR Belouizdad (Algeria), Algeria JS Kabylie (Algeria), Al Hilal (Sudan), Coton Sport (Cameroon), Al Merrikh (Sudan) na Vipers (Uganda).
Droo ya Makundi inatarajiwa kupagwa Mwezi Novemba Makao Makuu SHirikisho la soka Barani Afrika ‘CAF’.
Ikumbukwe kuwa, lengo kuu la Simba SC msimu huu 2022/23 katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ni Kucheza hatua ya Nusu Fainali na ikiwezekana Fainali.