Inaelezwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Simba SC, Juma Mgunda, amepewa jukumu jipya la kuiongoza Simba Queens, akichukua mikoba iliyoachwa na Mganda, Charles Lukula, imefaharmika.
Mgunda alikuwa Kocha Msaidizi wa Wekundu wa Msimbazi, lakini mabosi wa klabu hiyo wameamua kumpa majukumu mapya.
“Ni kweli kwa sasa kikosi cha timu ya wanawake amekabidhiwa majukumu Mgunda, atakuwa akifundisha timu hiyo huku akiendelea na majukumu yake mengine ya ufundi kwa timu zote za Simba,” kimesema chanzo chetu.
Simba Queens ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Masala Princess katika Tamasha la Simba Day ikiwa chini ya Kocha Msaidizi, Sophia Mwasikili.
Hata hivyo ilipotafutwa Meneja wa timu hiyo, Selemani Makanya, alisema bado hawajapewa taarifa rasmi kuhusu kocha anayechukua mikoba ya Lukula.
“Suala hili bado liko katika mikono ya viongozi, wameniambia tayari kocha ameshapatikana na ataanza majukumu yake baada ya kuanza kambi hivi karibuni,” amesema meneja huyo.
Ameongeza wamefanya usajili mzuri kwa kuongeza nguvu katika kikosi chao kwa kuzingatia mapungufu walioyabaini katika msimu uliomalizika.
Amewataja wachezaji wapya waliosajiliwa ni Isabelle Diakiese kutoka Bikira FC ya DRC, Ritticia Nabbosa wa Fountain Gate Princess na Joanitha Ainembabazi aliyekuwa Ceasiaa Queens.