Kocha Msaidizi wa Simba SC Juma Mgunda amezungumzia maneno yanayotembea mitandaoni kwamba sio sehemu ya kikosi kipya cha Mnyama kwa msimu ujao wa 2023/24.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Kocha Robertinho kuwaambia Viongozi wa Simba SC wampe mkataba Mnyarwanda Hategekimana Corneille wa Rayon Sports kama kocha wa viungo lakini awali akiwa naye Rwanda akimtumia kama mshauri wake.
Mgunda ambaye ni mzoefu na miongoni mwa makocha wazawa wasomi akiwa na leseni A ya CAF, amesema kuwa bado yupo sana Simba SC, akizikana tetesi za kutaka kurejea kwenye timu yake ya zamani Coastal Union ya Tanga.
Amefafanua kwamba Coastal licha ya kuwa washikaji zake, lakini ana matatizo nao binafsi ambayo hakutaka kuyaweka wazi.
Kocha huyo ambaye kwa sasa yupo mapumzikoni Tanga baada ya kumalizika msimu wa Ligi Kuu Bara, amesema ataendelea kuwatumikia wana Msimbazi hadi mkataba wake utakapomalizika ndipo atakapojua kinachofuata na bosi wake, Robertinho hajamwambia kama kuna mabadiliko yoyote ya kibarua chake.
“Mmefanya vizuri kuniuliza, kwani majibu yangu yatawapa kujua bado ni mfanyakazi wa Simba SC. Kuhusu Coastal siwezi kukataa kwamba ni timu yangu ambayo nimetoka nayo mbali, tukirekebisha matatizo yetu tutaendelea salama,” amesema kocha huyo ambaye amejiwekea rekodi nzuri Simba SC.
“Nipo Tanga kwa mapumziko utakapofika muda wa kurejea kwenye majukumu Simba SC mashabiki wangu wataniona,” amesema na kuongeza kuwa msimu uliomalizika aliuona ushindani mkubwa ambao unawapa picha ya kufanya maandalizi makubwa zaidi kwa ajili ya ujao.
“Ligi ina ushindani mkali na soka linakuwa, hivyo kila timu itakuwa inajipanga kulingana na mahitaji yake ya msimu mwingine,” amesema Mgunda ambaye ana mchango mkubwa Simba SC akiivusha kipindi anakaimu ukocha mkuu baada ya kuondoka Zoran Maki na kutengeneza timu bora iliyoshinda mechi nyingi za Ligi Kuu kufanya vizuri kimataifa.