Wakati Uongozi wa Simba SC ukidhamiria kuboresha Benchi la Ufundi la Timu ya Wakubwa ya Wanaume, inadaiwa kuwa Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Juma Mgunda huenda akachukua nafasi ya Charles Lukula aliyekuwa akikinoa kikosi cha Simba Queens.
Simba Queen inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, ambayo msimu huu imemaliza nafasi ya pili na kushindwa kutetea taji lao la ubingwa, hivi karibuni uongozi wa klabu hiyo ulitangaza kuachana na kocha Lukula pamoja na makocha wengine wa timu ya wanaume wakiwamo kocha wa makipa Chlouha Zakaria, wa viungo, Kelvin Mandla na mchua misuli, Fareed Cassiem.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Simba SC, zimeeleza kuwa Mgunda ataendelea kusalia ndani ya Wekundu wa Msimbazi hao kwa kupewa jukumu la kukinoa kikosi cha timu ya wanawake kwa msimu ujao.
Taarifa hizo zimetanabaisha kuwa hiyo ndiyo mipango ya Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo baada ya kukutana juma lililopita huku kocha wa viungo wa timu ya wanaume, Simba akitajwa kuwa atakuwa ni yule wa Vipers FC ya Uganda, Raia wa Rwanda, Hategekimana Corneille, ambaye atatua kuchua nafasi ya Kelvin.
Kwa upande wa Mgunda amesema bado yupo sana Simba na sasa yuko kwenye mapumziko baada ya msimu wa 2022/23 kumalizika hivi karibuni.
“Bado ni mfanyakazi wa Simba na sasa niko Tanga baada ya mapumziko na muda utakapofika nitarejea kwenye majukumu yangu Simba,” amesema kocha huyo
Hata hivyo Meneja wa timu ya Simba Queens, SelemanĂ Makanya, ambaye amesema hata yeye amekuwa akizisikia tetesi za Mgunda kuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo kuchukua mikoba ya Lukula, lakini hajapewa taarifa rasmi.
“Bado sijapewa taarifa zozote kuhusu kocha mkuu maana ninachojua uongozi uko kwenye mchakato, kuhusu Mgunda hata mimi nimesikia hivyo, kuwa anakuja kwenye timu yetu ila bado sina taarifa kamili na ninaimani viongozi wa najua nini wanafanya kwenye maboresho ya mabenchi ya ufundi ikiwamo la kwetu la Simba Queens,” amesema meneja huyo.