Kocha Msaidizi wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema, baada ya kuambulia matokeo ya 1-1 dhidi ya Namungo FC jana Jumatano (Mei 03), kwa sasa nguvu kubwa wameziweka katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Simba SC itacheza dhidi ya Azam FC Jumapili (Mei 07) katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, na mshindi wa mchezo huo atatinga Fainali ya ASFC msimu huu 2022/23.
Mgunda ameweka wazi kuwa: “Tumemaliza mchezo wetu dhidi ya Namungo FC, wachezaji wetu wote wapo katika hali nzuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Azam FC Jumapili, tunaamini tutapambana na kupata ushindi.”
“Uzuri ni kwamba wachezaji wote wapo tayari na wanatambua kwamba kuna kazi ya kufanya, yaliyopita hayo yamepita, sasa nguvu kubwa ni kutafuta ushindi kwenye mchezo wetu na Azam FC, ili tupate nafasi ya kufika Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.”
Hivi karibuni, Simba SC imetoka kufungashiwa virago na Wydad Casablanca ya Morocco kwenye hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Simba SC yaapa kuiharibia Young Africans
Katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC imeshacheza michezo 27 ikifikisha alama 64, huku vinara Young Africans wakiwa na alama 68 wakicheza michezo 26.
Young Africans baadae leo Alhamis (Mei 04) itacheza mchezo wake wa 27 dhidi ya Singida Big Stars itakayokuwa nyumbani katika Uwanja wa CCM Liti, mjini Singida.