Mkuu wa Benchi la Ufundi Simba SC Juma Mgunda amesema, hana budi kusahau yaliyopita na kuelekeza nguvu zake katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utamkutanisha na Young Africans.
Simba SC iliyopoteza Ubingwa wa Tanzania Bara msimu uliopita, itacheza dhidi ya Young Africans Jumapili (Oktoba 23), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, ikiwa mgeni katika mchezo huo.
Kocha Mgunda amesema anaamini wachezaji wapo tayari, huku akiwa na matumaini watapambana katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa Soka nchini Tanzania.
Amesema Kikosi chake kitaingia Uwanja kikiwa na Morali ya juu, baada ya kupata matokeo mazuri kwenye michezo iliyopita, hivyo atahakikisha anawaandaa vizuri wachezaji wake ili wakatimize jukumu la kuwapa furaha mashabiki wa Simba SC.
“Tumerejea uwanjani kujiandaa na mchezo wetu ujao, tunayafanya kazi mapungufu yetu ya mchezo uliopita. Tunatambua mchezo ujao utakuwa na ushindani mkubwa, wachezaji wanatambua umuhimu wa kila mchezo ulio mbele yetu.”
“Tunaenda kucheza kila mchezo tukiingia kwa tahadhari kubwa kwa kuwaheshimu wapinzani wetu, kila mchezaji anatambua umuhimu wa mchezo wetu ujao ili kufikia malengo ya kufanya vizuri kwenye Ligi ya ndani na Michuano ya Kimataifa.”
Kuhusu wachezaji wake, Kocha Mgunda amesema kila mchezaji kwenye kikosi cha Simba SC ana umuhimu na amekuwa akiwahimiza kuwa tayari kucheza muda wowote.
“Kwangu hakuna huyu mchezaji wa kocha, kila mchezaji aliyekuwa kwenye timu wote ni wangu na kila mmoja anatakiwa kujiandaa muda wowote kucheza na kutafuta matokeo mazuri kwa klabu.” amesema Mgunda
Mchezo wa Jumapili (Oktoba 23) utakua wa Kwanza kwa Kocha Juma Mgunda kukutana na Young Africans tangu alipotangazwa kukaimu nafasi ya Kocha Mkuu Simba SC mwanzoni mwa msimu huu, baada ya kuondoka kwa Kocha Zoran Maki.
Simba SC imekua na matokeo mabaya dhidi ya Young Africans kwa siku za karibuni, baada ya kukubali kupoteza katika mchezo wa Ngao ya Jamii kwa kufungwa 2-1 jijini Dar es salaam, na kabla ya hapo ilipoteza kwenye mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho kwa kufungwa 1-0 jijini Mwanza.
Hata hivyo msimu uliopita 2021/22, Miamba hiyo ya Soka la Bongo haikufungana ilipokutana kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hadi sasa Simba SC inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanznaia Bara ikiwa na alama 13 sawa na Young Africans, lakini Mnyama ana uwiyano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.