Kocha Msaidizi wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema kikosi chao kimejipanga kucheza dhidi ya Young Africans kama fainali kwa sababu ndio utakaoamua hatima ya kuendelea katika mbio za ubingwa kwa upande wao.
Simba SC itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kesho Jumapili (April 16), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kuanzia saa 11 jioni.
Mgunda amesema kikosi chao kilianza mazoezi mara baada ya kumaliza mchezo dhidi ya Ihefu FC mwanzoni mwa juma hili, kwa sababu walifahamu wanahitaji kuwa imara zaidi katika kila eneo.
“Siyo kama tulianza maandalizi juzi, tulikuwa tunaijua, na tarehe inafahamika kwa hiyo mchezo huu tumejiandaa muda mrefu tu, hiki unachokiona ni tunakamilisha tu maandalizi ya mwisho ya mchezo. Tunaweza kusema mchezo ni mzito, tunaweza kusema una hatima yetu.”
“Vile vile kwa sababu bado tuko kwenye mbio za ubingwa na mimi huwa kila siku nasema ‘haiwi mwisho hadi iwe mwisho’, bingwa atapatikana baada ya ligi kumalizika. Tunauchukulia mchezo huu kwa umuhimu wa kipekee kabisa,” amesema Mgunda ambaye aliongoza kikosi cha Simba SC katika mchezo wa Mzunguuko wa kwanza na kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Young Africans
Katika mchezo huo Young Africans inajivunia ubora wa wachezaji wake wakiongozwa na Stephane Aziz Ki aliyefunga bao la kusawazisha kwenye mchezo uliyopita, Fiston Mayele Mshambuliaji tegemeo wa kikosi hicho, lakini pia wapo mawinga hatari kama Jesus Moloko na Tuisila Kisinda huku idara ya ulinzi ikiongozwa na Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Djuma Shaaban.
Simba yenyewe itashuka katika dabi hiyo ikimtumia kwa mara ya kwanza ni Jean Baleke, Mshambuliaji wa kumainiwa kwa sasa na timu hiyo, Saido Ntibazonkiza ambaye ameshawahi kucheza dabi, lakini itakuwa ni ya kwanza akiwa na Wekundu wa Msimbazi pamoja na nyota, Clatous Chama, Pape Sakho na Kibu Denis.
Hadi sasa Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 68, huku Simba SC ikishika nafasi ya pili kwa kumiliki alama 60 na timu zote zimeshacheza michezo 25.