ANAANDIKA MASSAU BWIRE.
Ni Jumapili nyingine ya kipekee katika historia ya maisha yako, April 17, 2022, Jumapili ya Pasaka, siku ambayo Wakristo kote Duniani, wanasherehekea kumbukizi ya kufa na kufufuka kwa Masihi, Yesu Kristo, aliyekufa kwa ajili ya ukombozi wa maisha yao.
Ni Jumapili ya kipekee mno, ambayo ndugu zetu, rafiki zetu, wenzetu Waislamu, wakiendelea na mfungo wao wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wanafanya mashindano makubwa ya kusoma Quran katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar Es salaam.
Kama kwamba hiyo haitoshi, Jumapili ya leo, ni ya kipekee sana katika historia ya mafanikio ya klabu ya Simba SC katika soka la Afrika, inakwenda kukutana na klabu ya Orlando Pirates kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, mchezo wa awali katika kinyang’anyiro cha kombe la Shirikisho barani Afrika hatua ya robo fainali, kuwania kufuzu hatua ya nusu fainali.
Ni Jumapili ambayo, kwa mara ya kwanza VAR, inatumika katika uwanja wa Benjamin Mkapa na Tanzania kwa ujumla wake, Jumapili muhimu sana, ya kukumbukwa mno katika historia ya soka letu, ndani ya nchi yetu.
Jumapili hii, nyeti namna hii katika historia hii, tusiiangushe, tuipambe, tuilembe Watanzania, iondoke na shamrashamra, ikituachia nderemo na furaha tele.
Furaha yetu Watanzania kwa Jumapili hii ya kihistoria, ni kuishuhudia Simba SC, Wekundu wa Msimbazi ikiibuka na ushindi wa kishindo dhidi ya mpinzani wake Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Shime Watanzania wenzangu, wazalendo, wafia nchi, kwa umoja wetu, twendeni kwa wingi, tukaujaze uwanja wa Benjamin Mkapa, tukawashangilia Watanzania wetu, Simba SC, tuchagize ushindi wao katika mchezo huo wa kihistoria katika siku hii, Jumapili ya kihistoria, na kuifanya Jumapili hii kuwa ya kihistoria zaidi katika maisha yetu ya kisoka.
Mungu ibariki Simba SC, Mungu ibariki Tanzania.
Simba SC nguvu moja.
Masau Kuliga Bwire – Mzalendo