Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesajili na kuwapatia Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) jumla ya walipakodi 676 wakati wa Kampeni ya utoaji Huduma, Elimu na
Usajili wa walipakodi iliyomalizika hivi karibuni mkoani Njombe.
Akizungumza wakati wa kufunga kampeni hiyo mkoani humo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Njombe kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha hadi kufikia kusajili idadi hiyo ya walipakodi.
“Kwa dhati kabisa, nachukua fursa hii kuushukuru uongozi wa hapa mkoani Njombe kwa maana ya Mkuu wa Mkoa na watendaji walio chini yake kwa ushirikiano mkubwa waliotuonyesha katika kampeni hii mpaka tumefanikiwa kusajili jumla ya walipakodi 676 ambao wote tumewapatia Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi” amesema Kayombo.
Kayombo alisema kuwa, idadi hiyo inaipa nguvu Mamlaka ya kuendelea na zoezi hilo katika Mikoa ambayo inapata shida ya kupata huduma za TRA kwa wakati.
Aidha, Mkurugenzi Kayombo ametoa wito kwa wananchi wa Njombe na Wilaya zake za Njombe Mjini, Makete, Makambako, Ludewa na Wanging’ombe kutembelea ofisi za TRA mkoani hapa hata mara baada ya zoezi hili kumalizika kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali pamoja na elimu ya kodi.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Wilaya ya Matamba, Bina Nyagawa ameishukuru TRA kwa zoezi hili la kutoa huduma, elimu na kusajili walipakodi kwani walipakodi wengi wamekuwa wakitumia muda mrefu na gharama kubwa kwenda kupata huduma ya TIN jambo ambalo liliwafanya baadhi ya walipakodi hususani wafanyabiashara hao kuendelea kufanya biashara zao bila kusajiliwa na TRA.
“Tunashukuru sana kwa ujio wa zoezi hili mkoani kwetu kwasababu limewarahisishia wafanyabiashara wengi muda na gharama za kufuatilia huduma ya TIN ambayo inapatikana Njombe Mjini” ameeleza Nyagawa.
Bina Nyagawa ameiomba TRA kutembelea Mkoa wa Njombe na kufanya kampeni hiyo mara kwa mara kwa kuwa kila siku wanaibuka walipakodi wapya ambao wanatakiwa kupewa elimu ya kodi ili waweze kuchangia mapato ya Serikali.
Kampeni ya utoaji Huduma, Elimu na Usajili wa walipakodi mkoani Njombe ilianza tarehe 18 hadi 23 Juni, 2018 ikiwa na lengo la kufikia Mikoa na Wilaya zote ambazo zina changamoto ya kupata huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.