Jumuiya ya Taasisi za Kiislam zimepinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutangaza marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliopangwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.

Katibu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Issa Ponda amesema kuwa uamuzi huo wa ZEC sio sahihi na kwamba pande zote mbili zinapaswa kuendelea na mazungumzo na kutoa kauli ya pamoja kuhusu kukubaliana au kutokubaliana.

“Utaratibu ule ulikuwa ni mzuri wa mazungumzo. Kwa msingi huo tunataka ule utaratibu ufike mwisho. Na kufika mwisho kwa ule utaratibu ni kuhakikisha kwamba inatoka kauli ya pamoja ya pande zote mbili zilizokuwa katika mazungumzo,” alisema Sheikh Ponda.

“Aidha kauli hiyo iwe ni kauli ya kukubaliana au kutokubaliana. Lakini kimsini iwe ni kauli ya pamoja. Hivyo ndivyo inavyokuwa mazungumzo ya viongozi… ya watu wenye busara kwamba mnafika pahala mnatoa tamko la pamoja,” Katibu huyo wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu alifafanua.

Sheikh Ponda alieleza kuwa hakuna sababu ya kurudia uchaguzi ikiwa waangalizi wote wa kimataifa walitoa ripoti zao zinazoonesha kuwa uchaguzi ulikuwa huru na haki.

Jumuiya hiyo imekosoa kauli za baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa waliojitokeza na kueleza kuwa uchaguzi utarudiwa wakati mazungumzo yakiendelea.

Kauli ya Jumuiya hiyo ya Kiislamu inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) kuunga mkono uamuzi wa kurudia uchaguzi wa Zanzibar.

 

Hatari: Virusi vya 'ZIKA' huambukizwa kwa njia ya 'Kujamiiana'
Mwalimu aishi darasani miaka 10 kushinikiza alipwe stahiki zake