Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp sio tu kwamba alikuwa na sababu ya kulala na tabasamu lake baada ya kuifungashia vilago Manchester City kwa kipigo cha 2-1, bali pia alishangazwa na kupigwa kwa Barcelona.
Usiku wa jana ulikuwa wa aina yake kwenye Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ambapo Roma iliigalagaza Barcelona kwa kipigo cha 3-0, Stadio Olimpico.
Klopp alisema kuwa baada ya kupokea ushindi wa timu yake dhidi ya Manchester City, alipata taarifa jinsi Barcelona walivyonyong’onyezwa na alidhani taarifa hiyo ilikuwa ni ‘utani’.
“Mimi niliambiwa na mtu nilipokuwa napanda ngazi kwenda kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi yetu. Kwakweli nilidhani ulikuwa utani tu. Sio kwamba naidharau Roma, la hasha, ni timu nzuri lakini sikutegemea,” alisema Klopp.
“Sikutegemea Barcelona ingeshindwa mechi ile, lakini nilijua inawezekana pia. Mwanzo nilijua fainali ingekuwa kati ya Manchester City na Barcelona, lakini sasa wote wametolewa,” aliongeza.
Hata hivyo, alisema kuwa hajali nani atakuwa nusu fainali, anachojali wao wako hapo na watafanya wanachotakiwa kufanya.
Alisema huu ni muda wa Liverpool kushinda kwani “Barca, Bayern, Real Madrid wamekuwa wakishinda kila kitu kwa miaka 20 sasa.”
Katika mchezo wa jana, Gabriel Jesus alianza kuwavuruga Liverpool kipindi cha kwanza hata kabla hawajatoa jasho lakini katika kipindi cha pili, Mohamed Salah na Roberto Firmino waliwainua Liverpool na kuwapa ushindi mnono unaowafanya kuwa na ushindi wa 5-1.