Meneja wa kikosi cha Liverpool Jurgen Klopp amesema bado yupo sana na hana mpango wa kuondoka klabuni hapo japokuwa wanapitia katika kipindi kigumu kutokana matokeo wanayoyapata msimu huu wa Ligi Kuu ya England.
Mameneja Brendan Rodgers na Graham Potter walishatimuliwa mwishoni mwa juma lililopita na kufanya idadi ya mameneja waliofukuzwa kabla ya kumalizika kwa msimu huu kufikia 12.
Katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, Liverpool ipo nafasi ya nane ikiwa na alama 42 ilizozivuna katika michezo 27 ilizocheza kabla ya mchezo wa dhidi ya Chelsea.
Meneja huyo kutoka nchini Ujerumani amesema hana mpango kuondoka kwa sasa ndani ya kikosi hicho japokuwa wamekuwa wakipitia changamoto ya kukosa matokeo mazuri.
“Kama ungekuwa msimu wangu wa kwanza kuinoa Liverpool, ningeweza kufanya maamuzi mengine.”
“Ninatarajia kuendelea kuwepo kutokana hapa kutokana na mazuri niliyoyafanya hapo awali, sitaondoka kwa sababu ya kufanya vibaya msimu huu,” amesema.
Klopp mwenye umri wa miaka 55, tayari aliishaipatia Liverpool mafanikio makubwa ikiwemo kubeba mataji katika kipindi cha miaka saba na nusu aliyokaa Anfield ambapo timu ilipoteza michezo mitatu ya mwisho katika michuano yote.
“Tuna wamiliki ambao wanatambua ugumu wa matokeo ambayo tunayapitia kwa sasa, haina haja ya kuanza kujilaumu, nina imani tutafanya vizuri zaidi msimu ujao.”
“Ninatambua nitaendelea kuwepo katika kikosi cha Liverpool kutokana na kilichotokea hapo awali,” amesema.