Mabingwa watetezi wa michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya Liverpool, wameanza vibaya msimu huu, kwa kukubali kufungwa na SSC Napoli waliokua nyumbani mjini Naples-Italia usiku wa kuamkia leo.

SSC Napoli inayonolowa na Carlo Anceloti, ilijinyakulia ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya majogoo hao wa Liverpool, yaliyofungwa na Dries Mertens kwa mkwaju wa penati dakika ya 82, huku Fernando Llorente akishindilia msumari wa pili dakika ya 90.

Kufuatia kichapo hicho, meneja wa mabingwa hao wa barani Ulaya Jurgen Klopp, alijitetea katika mkutano na waandishi wa habari kwa kusema kikosi chake kinapaswa kujilaumu kwa kushindwa kufikia lengo la kupata ushindi katika mchezo huo wa ufunguzi.

Klopp alisema washambuliaji wake hawakucheza kwa nidhamu, hali iliyowasababishia kukosa kujiamini pindi walipofika kwenye eneo la hatari la wapinzani wao.

Alisema nafasi nyingi walizopata washambuliaji wake zingeipa Liverpool ushindi katika mchezo huo wa Kundi E.

“Tumeshindwa wenyewe hakuna wa kumlaumu, tulipata nafasi nzuri za kufunga, lakini tulishindwa.

“Ulikuwa mchezo wa wazi na kila timu ilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda, lakini umaliziaji wetu haukuwa mzuri,”alisema Klopp.

Katika hatua nyingine meneja huyo alidai hakubaliani na penati ya SSC Napoli akidai haikuwa sahihi.

Hata hivyo meneja huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ya Ujerumani alisema ameridhika na kiwango cha wachezaji wake kwa sababu walitengeneza nafasi za mabao licha ya kutopata ushindi.

Kwa upande wa meneja wa SSC Napoli, Carlo Ancelotti alisema mbinu zake zilifanikiwa kwa kiasi kikubwa na kufanikiwa kuiangusha miamba ya soka kutoka nchini England.

Ancelotti alisema aliwapa maelekezo mabeki wake kucheza kwa nidhamu na mbinu kali ambazo zilizaa matunda, kwani beki wa kati Kalidou Koulibaly alikuwa nyota wa mchezo.

Matokeo ya michezo mingine ya ligi ya mabingwa barani Ulaya iliyochezwa usiku wa kuamki leo:

Kundi E

Salzburg 6 – 2 KRC Genk

 

Kundi F

Inter Milan 1 – 1 Slavia Prague

Borussia Dortmund 0 – 0  FC Barcelona

 

Kundi G

Olympic Lyon 1 – 1 Zenit St. Petersburg

Benfica 1 – 2 RasenBallsport Leipzig

 

Kundi H

Ajax 3 – 0 Lille

Chelsea 0 – 1 Valencia

Ligi ya mabingwa Ulaya kuendelea leo
Ross Barkley ajitwisha mzigo wa lawama, Lampard amtetea