Meneja wa majogoo wa jiji (Liverpool) Jurgen Klopp anategemea kuhamisha uhusiano uliopo kwenye safu ya ulinzi ya timu ya taifa ya Croatia na kupeleka Anfield, kwa kumsajili Domagoj Vida.
Klopp ameeleza mpango wa kutaka kumsajili beki huyo, baada ua kuridhishwa na uwezo wake aliouonyesha wakati wote wa fainali za kombe la dunia, zinazendelea nchini Urusi.
Vida mwenye umri wa miaka 29 amekua na uhusiano mzuri wa kiuchezezaji na beki wa Liverpool Dejan Lovren, katika timu ya taifa ya Croatia ambayo juma hili itacheza mchezo wa nusu fainali dhidi England.
Klopp aliibua hisia na kutangaza dhamira yake ya kutaka kumsajili beki huyo, baada ya mchezo wa robo fainali kati ya Croatia na wenyeji Urusi, ambao ulimalizika kwa changamoto ya mikwaju ya Penati.
Hata hivyo mpaka leo jumatatu, bado hakuna taarifa zozote za klabu ya Liverpool kuwasilisha ofa kwenye klabu ya Besiktas ya nchini Uturuki, kwa ajili ya uhamisho wa beki huyo.
Vida bado ana mkataba wa miaka minne wa kuitumikia Besiktas, na taarifa zinaeleza kuwa, huenda thamani yake ikawa juu katika kipindi hiki kutokana na kiwango kikubwa alichokionyesha kwenye fainali za kombe la dunia.