Meneja wa klabu ya Liverpool, Jurgen Klopp amesema anajua kwamba mashabiki wa klabu hiyo wana wasiwasi na hatma ya timu yao, lakini akasema watafurahi tu.

Kocha huyo raia wa Ujerumani amesema kwamba anakusudia kuisuka timu hiyo kuwa moja ya timu tishio barani Ulaya na hilo si jambo la kufanya kwa siku moja.

“Nimekuja hapa kuna wachezaji hawana msaada sana, wanajitahidi katika baadhi ya mechi lakini hawana uwezo katika mechi nyingine,” amesema na kuongeza.

“Sasa nafanya usajili wa maana zaidi ambao kila mmoja utamfurahisha, tunataka Liverpool iwe kali zaidi na hiyo ndiyo heshima na hisani nitakayowalipa mashabiki ambao ndio walishinikiza mimi niwe hapa.”

Liverpool wanataka kumsajili mchezaji wa Shakhtar Donetsk, Alex Teixeira mwenye asili ya Kibrazil na kama dili hilo litafanikiwa, huo utakuwa usajili mkubwa wa kwanza kufanywa na kocha Jurgen Klopp tangu awe bosi wa kikosi cha Liverpool.

Wekundu hao wapo tayari kulipa kiasi cha pauni mil. 24.5 kwa ajili ya kuinasa saini ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 26.

Klabu ya nyota huyo ambaye pia anahusishwa na Chelsea, imeweka dau la pauni mil. 36 kwa klabu inayotaka kumsajili mshambuliaji wao.

Klopp anataka kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kuwa washambuliaji wake wengi ni majeruhi kwa sasa, Danny Ings, Divock Origi pamoja na Daniel Sturridge wote wanauguza majeraha.

Usajili wa pauni mil. 32.5 kumnasa Christian Benteke umeshindwa kuzaa matunda yaliyotarajiwa baada ya timu hiyo kujikuta ikifunga mabao 25 katika mechi 22 za Ligi Kuu England hadi sasa.

Teixeira ameshatupia kabatini jumla ya magoli 22 kwenye mechi 15 za Ligi na magoli mengine 10 kwenye michuano ya Klabu Bingwa msimu huu.

Nyota huyo alianzia soka lake kwenye klabu ya Vasco da Gama ya Brazil kabla ya kuhamia Shakhtar mwaka 2010.

Klopp amemsajili kwa mkopo beki Steven Caurkel wa QPR na amekamilisha dili la kinda mwenye miaka 19, Marko Grujic kwa pauni mil. 5.1 abae ameachwa kwa mkopo kwenye klabu ya Belgrade hadi majira ya joto.

Usajili wa Teixeira utakuwa ni usajili wa kwanza mkubwa kwa Klopp kwenye soko la usajili na mshambuliaji huyo atakuwa ni Mbrazil wa nne kwenye kikosi cha Liverpool akiwa ametanguliwa na Lucas Leiva, Roberto Firmino na Fhilippe Coutinho.

Bale Akanusha Uvumi Uliosambwazwa Kwa Makusudi
Nemanja Vidic Avunja Ukimya