Meneja wa majogoo wa jiji Liverpool Jürgen Norbert Klopp, amekanusha taarifa za kumuweka sokoni kiungo mshambuliaji kutoka nchini Brazil Philippe Coutinho, ambaye anahusishwa na taarifa za usajili.

Magwiji wa soka nchini Hispania Real Madrid na FC Barcelona wanatajwa kuwa katika harakati za kumuwania kiungo huyo ambaye amekua msaada mkubwa kwenye kikosi cha Liverpool.

Klopp amesema taarifa za mchezaji wake kuhusishwa na usajili wa klabu hizo zinazoshiriki ligi ya nchini Hispania (La Liga), hazina ukweli wowote na anachokifahamu kwa sasa Coutinho ni mchezaji halali wa Liverpool.

Amesema taarifa za mchezaji huyo kutakiwa nchini Hispania huenda zikawa zimepikwa kwa makusudi ya watu wachache, lakini ukweli ni kwamba hatokua radhi kukubali jambo hilo litokee.

Hata hivyo ameonyesha kuridhishwa na kiwango cha Coutinho kwa msimu huu, na kusema huenda jambo hilo likawa ni sehemu ya sababu ambazo zimechangia mchezaji wake kuhusishwa na safari ya kuelekea nchini Hispania.

“Inafurahishwa kuona ama kusikia taarifa za Coutinho kutakiwa na FC Barcelona ama Real Madrid, naamini kiwango chake ndio sababu ya mambo yote kufikia hapa yalipo, lakini bado ninasisitiza sitokua tayari kuona hilo likitokea Anfield.

“Hatujawahi kuwa na mawazo ama mpango wowote wa kuuza mchezaji aliye kikosini kwa sasa, na hii inatokana na malengo tuliojiwekea kwa msimu huu ambao tunafahnya vizuri katika mbio za ubingwa.” Alisema Klopp

Coutinho mwenye umri wa miaka 24, alisajiliwa na Liverpool mwaka 2013, na tayari msimu huu ameshafunga mabao sita na kutoa pasi za mwisho 14.

Kufuatia hali hiyo, Coutinho amekua na mchango mkubwa wa kuifikisha Liverpool katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ya nchini England, kwa kumiliki point 44 zilizopatikana katika michezo 20 waliyocheza.

Kiti Cha Arsene Wenger Chamtesa Roberto Mancini
Olivier Giroud Awatoa Hofu Mashabiki