Meneja wa mabingwa wa soka barani Ulaya Liverpoool Jurgen Klopp, ametishia kutopeleka timu uwanjani, endapo chama cha soka nchini England (FA) hakitabadilisha ratiba ya mchezo wa robo fainali ya kombe la ligi (Carabao Cup).
Klopp alitoa kitisho hicho, mara baada ya kikosi chake kuisasambua Arsenal kwa mikwaju ya penati tano kwa nne, kwenye uwanja wa Anfield usiku wa kuamkia hii leo, kufuatia timu hizo kufungana mabao matano kwa matano katika muda wa dakika 90.
Meneja huyo kutoka nchini Ujerumani amesema kuna haja ya FA kufikiria upya ratiba ya mchezo wa robo fainali, ambayo dhahir itaingiliana na ratiba ya kikosi chake kwenda kushiriki michuano ya klabu bingwa duniani (FIFA Club World Cup) mwezi Disemba.
Ratiba ya mchezo wa robo fainali inaonyesha timu zilizofuzu hatua hiyo zitacheza kuanzia Disemba 17 na 18, huku Liverpool ikitarajia kuondoka juma hilo kuelekea kwenye michuano ya dunia.
“Hatuwezi kuwa waathirika wa tatizo hili,” alisema Klopp.
“Kama watashindwa kupanga ratiba vizuri ya robo fainali ya Carabao Cup kwa ajili yetu, sitopeleka timu uwanjani, ni bora wakaangalia upya namna ya kumaliza hili tatizo.”
“FIFA wameshatuambia ni lazima tuwe kwenye michuano ya klabu ndani ya muda maalum, huku FA wanaendelea kusisitiza ratiba ya ligi na michuano mingine ya ndani lazima ifuatwe.”
“Kama itaendelea kuwa hivi, ni vigumu kwa timu moja kukabiliwa na ratiba zaidi ya moja tena ya michuano tofauti, FA wanapaswa kujipanga upya na kuangalia wanalimaza vipi hili tatizo.”
“Lengo letu kubwa ni kushiriki michuano ya dunia na kutwaa ubingwa, hatutaki kuipoteza hiyo nafasi, naamini ratiba iliopo ingekua na nafasi kubwa endapo wapinznai wetu (Arsenal) wangepita, lakini imekua tofauti,” aliongeza meneja huyo mjerumani.
Kikosi cha Liverpool kinatarajiwa kuondoka England Disemba 16 kuelekea Qatar kwa ajili ya michuano ya klabu bingwa duniani, tarehe ambayo inaonyesha watapaswa kucheza mchezo wa robo fainali ya kombe la Carabao.