Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ametajwa kuwa mrithi sahihi wa Hansi Flick baada ya kutimuliwa katika timu ya taifa ya Ujerumani.
Uamuzi huo umefuata Ujerumani kupokea kichapo cha mabao 4-1 ilichopata Ujerumani katika mechi ya kirafiki dhidi ya Japan, mwishoni mwa juma lililopita.
Licha ya Klopp kuweka wazi kwamba atajitolea zaidi kuinoa Liverpool, lakini alikiri litakuwa jambo la kujivunia endapo atakifundisha kikosi cha Ujerumani ambako ndiko kwao.
“Kazi ya kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani ni jambo la kujivunia. Hakuna maswali kuhusu hilo, lakini siwezi kuondoka Liverpool kwa sasa halafu nikaifundishe kwa muda mfupi. Huwezi kufanya kazi kwa namna hiyo kama ikitokea natakiwa kuwepo muda wote kwa ajili ya timu.” alisema Klopp
Kabla ya kufukuzwa kazi, Hansi alisisitiza kwamba anastahili kupewa muda zaidi wa kukisuka kikosi chake baada ya kichapo walichopata dhidi ya Japan, lakini mashabiki wengi wa soka Ujerumani walionyesha masikitiko yao mitandaoni wakimtaka kuondoka.
“Mimi na benchi langu la ufundi tumejiandaa kwa kila kitu. Nadhani tunaendelea vizuri na maandalizi. Nastahili kuwa kocha, Japan ni timu nzuri tumesikitishwa na matokeo. Sasa tunatakiwa kuimarika zaidi kwa ajili ya mchezo unaofuata dhidi ya Ufaransa” amesema.
Ujerumani iliweka rekodi ya kufungwa mara tatu mfululizo katika mechi tano huku timu hiyo ikijindaa kuwa mwenyeji wa Euro mwakani.