Mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC watajaribu kutuma ofa ya kumsajili kiungo wa majogoo wa jiji Liverpool Emre Can.
Juventus watafanya hivyo, kwa kuamini huenda wakafanikisha kumsajili kiungo huyo kutoka nchini Ujerumani, kufuatia mkataba wake na Liverpool kuelekea ukingoni.
Mkataba wa Can utafikia kikomo mwishoni mwa msimu wa 2017/18, na pamekua hakuna dalili zozote za kuanza mazungumzo ya kusainishwa mkataba mpya huko Anfield.
Juventus wamejiandaa kutuma ofa ya Euro milioni 25 ambayo wanaamini itatosha kuushawishi uongozi wa Liverpool, ili ukubali kumuachia kiungo huyo ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Ujerumani kilichotwaa ubingwa wa kombe la Mabara kwa kuifunga Chile mapema mwezi huu kule nchini Urusi.
Hatua ya kutaka kutuma ofa ya kumsajili Can, inachukulia kama sehemu ya kujihami kwa viongozi wa Juventus, baada ya AC Milan kujitokeza hadharani na kutangaza mpango wa kutaka kumsajili Leonardo Bonucci.