Mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC wameitoa nishai AS Monaco ya Ufaransa kwa kuichapa mabao mawili kwa sifuri katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Mchezo huo ulichezwa usiku wa kuamkia leo kwenye dimba la Louis II huko jijini Monaco nchini Ufaransa.
Mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Lahoz kutoka Hispania, ulishuhudiwa Juventus FC wakipata mabao yao katika kipindi cha kwanza na cha pili, kupitia kwa mshambuliaji wao wa kimataifa kutoka nchini Argentina Gonzalo Higuain, katika dakika za 29 na 59.
Mabao yote yalitokana na krosi safi za mlinzi wa kulia kutoka nchini Brazil, Dani Alves aliyekuwa akipanda mara kwa mara kusaidia mashambulizi.
Ushindi huo muhimu umeiweka Juventus katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya fainali, kabla ya kumaliza dakika nyingine 90 za mchezo wa mkondo wa pili ambao utachezwa juma lijalo mjini Turin nchini Italia.
Wababe hao wa soka katika ligi ya Sirie A, watahitaji matokeo ya ushindi wowote ama sare, ili waweze kukata tiketi ya kuelekea jijini Cardiff nchini Wales ambapo mchezo wa fainali utachezwa kwenye uwanja wa Millennium.