Beki kutoka nchini Italia Leonardo Bonucci huenda akarejea kwa mabingwa wa soka nchini humo Juventus FC, akitokea AC Milan baada ya kuitumikia klabu hiyo ya mjini Milan kwa mwaka mmoja.
Matarajio ya beki huyo mwenye umri wa miaka 31 kurejea Allianz Stadium, yameanza kuonyesha dalili, kufuatia mazungumzo yanayoendelea baina ya mmiliki wa klabu ya AC Milan Yonghong Li na mtendaji mkuu wa Juventus Paratici.
Mmiliki wa AC Milan anaamini mazingira ya soka la Juventus huenda yakampa furaha Bonnucci ambaye msimu uliopita alishindwa kufikia lengo la kutwaa taji, akiwa na The Rossoneri (The Red and Blacks).
Beki huyo aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema, hakutarajia kama mambo yangekua magumu AC Milan, na endapo atapata ofa ya kuondoka klabuni hapo itakua heri kwake, ili akajaribu mahala pengine.
Hata hivyo tatizo la uchumi linaloiandama klabu ya AC Milan katika kipindi hiki, nalo linatajwa kuwa sababu ya mmiliki wa klabu hiyo Yonghong Li kuwa tayari kufanya biashara ya kumuuza Bonucci, ili kufidia baadhi ya changamoto zinazoikabili klabu yake.
Klabu nyingine zilizoonyesha nia ya kumsajili Bonucci ni Manchester United ya England na Paris Saint-Germain ya Ufaransa, na tayari wakala wa beki huyo amesharipotiwa kukutana na mmiliki wa PSG mara kadhaa.
Taarifa zaidi zinasema, huenda mshambuliaji Gonzalo Higuain akatumika kama chambo ili kufanikisha harakati za kurejeshwa kwa Bonucci huko Allianz Stadium.
Huguain amekua katika harakati za kuuzwa na Juventus, baada ya kusajiliwa kwa mshambuliaji kutoka nchini Ureno Cristiano Ronaldo.