Klabu ya Soka ya Italia, Juventus itamrejesha uwanjani Cristiano Ronaldo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuitumikia timu hiyo kwenye mechi ya Series A, Udinese, Jumamosi hii.

Ronaldo ambaye amekana vikali tuhuma za kumbaka Kathryn Mayorga katika hotel ya Las Veras mwaka 2009, amekuwa akisikitikiwa na baadhi ya mashabiki wake wanaodai kuwa huenda tuhuma hizo zikamuathiri kisaikolojia na hivyo kuathiri kazi yake uwanjani.

Mchezaji huyo kutoka Ureno aliukosa mchezo wa Ligi ya Mabingwa wakati Juve ilipojitwalia ushindi dhidi ya ‘Young Boys’, kufuatia kuondolewa kwake mchezoni dhidi ya Valencia.

Hata hivyo, Bosi wa Juventus, Massimiliano Allegri amesema kuwa pamoja na mambo yanayoendelea dhidi yake, anamfahamu Ronaldo kuwa yuko tayari kurejea uwanjani na kwamba siku zote anabaki kuwa mchezaji mweledi.

“Nimemfahamu Cristiano kwa miezi mitatu sasa na kwa zaidi ya miaka 15 ya kazi yake ameonesha kuwa ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na mweledi akiwa ndani au hata nje ya mchezo,” alisema Allegri.

Bosi huyo wa klabu hiyo ya Italia iliyomnasa Ronaldo kwa donge la £99.2milioni mwezi Julai mwaka huu, alisema kuwa mchezaji huyo ana upeo mkubwa hivyo anaweza kujikita katika mchezo.

Tuhuma za ubakaji dhidi ya Ronaldo zimevivuta vyombo vya usalama ambavyo vimetangaza kuanza kufanya uchunguzi.

CR7 hatakuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ureno katika michezo dhidi ya Poland na Scotland.

Makampuni ya Nike na EA Sports yenye mkataba wa mabilioni ya shilingi na mchezaji huyo yamesema kwa nyakati tofauti kuwa yanafuatilia kwa ukaribu mwenendo wa tuhuma dhidi yake.

Mwanasheria wa mchezaji huyo amesema kuwa wanapanga kufungua kesi dhidi ya jarida la Ujerumani la ‘Der Spiegel’ lililochapisha tuhuma hizo kwa mara ya kwanza.

Mahakama yatoa hukumu kesi ya 50 Cent dhidi ya Rick Ross
Unafanya nini ukiwa na bosi mdogo kwako? Mambo 6 ya kuzingatia