Klabu ya Italia ya Juventus imesema kuwa inaendelea kumsaka aliyekuwa kiungo mchezeshaji wa timu hiyo, Paul Pogba ambaye hivi sasa anapiga soka kwenye klabu ya Manchester United kwa donge nono.
Klabu hiyo inayoongoza Serie A inaamini kuwa wanayo nafasi ndogo ya kufanikisha azma yao ya kumnasa mchezaji huyo wa Timu ya Taifa ya Ufaransa mapema Januari mwakani, kwani kufanikiwa kwao katika hilo kunategemea matakwa ya meneja mpya atakayepewa mkataba rasmi kukinoa kikosi cha Manchester United.
Endapo meneja mpya wa Wekundu wa Old Trafford ataonesha nia ya kutomhitaji Pogba, itakuwa rahisi kwa Juventus kufanikisha kumrejesha kikosini katika kipindi cha kiangazi kwani suala la bajeti ya kumg’oa Old Trafford, pamoja na mambo mengine bado ni mtihani.
Mwezi uliopita, wakati wa mvutano uliokuwa unatajwa kuwepo kati yake na aliyekuwa meneja wa Man United, Jose Mourinho, Pogba alidaiwa kuwaambia rafiki zake kuwa amepata ushawishi wa kurejea Italia, akiipa kipaumbele Juventus.
Aidha, Mtendaji Mkuu mpya wa Inter Milan, Beppe Marotta anadaiwa kuwa na nia ya kumnyakua Pogba. Marotta ambaye amewahi kuitumikia Juventus ana uhusiano mzuri na Pogba pamoja na wakala wake, Mino Raiola. Hali inayowapa wengi matumaini kuwa ana nafasi nzuri ya kumshawishi mchezaji huyo atakapofanya maamuzi ya kurejea Italia.
Bado ni kitendawili kizito kukitegua, kumuondoa Pogba Man United kutokana na mazingira ya kimkataba na donge nono kwenye maandishi ya mkataba huo.