Mabingwa wa soka nchini Italia, Juventus FC wamekiongezea makali kikosi chao tayari kwa msimu mpya wa Seria A baada ya kutangaza kumsajili winga kutoka nchini Brazil, Douglas Costa kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea Bayern Munich ya Ujerumani.

Costa mwenye umri wa miaka 24, amejiunga na Juventus ikiwa ni muda mfupi tangu Bayern Munich itangaze kumsajili kiungo wa kimataifa wa Colombia, James Rodriguez kutoka Real Madrid ya Hispania kwa mkopo wa misimu miwili.

Aidha, Juventus watalazimika kuilipa Bayern Munich kiasi cha Euro Milioni 6 kama ada ya kumsajili Costa kwa mkopo huo wa msimu mmoja, kisha wataongeza Euro Milioni 1 zaidi ikiwa watatwaa mataji msimu huu.

Wakati huohuo Juventus wamepewa nafasi ya kumsajili moja kwa moja Costa mwishoni mwa msimu ujao kwa ada ya Euro milioni 40 itakayolipwa katika kipindi cha miaka miwili.

Costa alianzia soka lake kwenye klabu ya Gremio ya nyumbani kwao Brazil kabla ya Januari 2010 kujiunga na Shakhtar Donetsk ya Ukraine ambayo alidumu nayo kwa misimu mitano na kuhamia Bayern Munich Agosti 2015.

Akiwa na Bayern Munich, Costa alifanikiwa kuifungia miamba hiyo ya Bavaria mabao 14 katika michezo 76 aliocheza.

Usher Raymond ndani ya Serengeti Tanzania
Ambwene Yessaya (AY) amvisha pete Remy