Mkali wa RnB, Juma Jux amesema kuwa maisha ya misukosuko na utulivu wa uhusiano wa mapenzi kati yake na Vanessa Mdee ni sehemu ya albam mpya ya msanii huyo wa kike iliyobatizwa jina la ‘The Money Mondays’.

Akizungumza na Dar24 kwenye hafla ya kusikiliza albam hiyo (Listening Party) jana usiku jijini Dar es Salaam, Jux alisema kuwa Vanessa amepitia maisha mengi wakati wa kuandaa albam yake hiyo na kwamba yeye ni sehemu ya maisha hayo, hivyo yatasikika ndani ya albam hiyo.

“Vanesa alipitia vitu vingi sana, na mimi pia naweza kusema nilikuwa katika maisha yake. So, maswali yako nadhani yatajibiwa kwenye ‘Money Mondays’. Kuna kitu ambacho ukikisikia kama ulikuwa unatufuatilia utajua hiki ni kitu fulani,” Jux aliiambia Dar24.

Jux na Vanessa walikuwa katika misukosuko ya penzi na kufikia hatua ya kuachana.

‘Kisela’ aliyowashirikisha P-Square ni moja kati ya nyimbo ambazo zimebeba ujumbe unaoaminika kuwa Vanessa alifanya kutokana na kilichokuwa kinaendelea kati yao.

Hata hivyo, wawili hao walirudisha kwa kasi penzi lao mwezi uliopita na huenda kuna kikubwa zaidi kinachokuja, kwa mujibu wa Jux aliyesisitiza kuwa hajutii yaliyotokea.

‘Listening Party’ ya The Money Mondays ilikuwa na ugeni maalum wa msanii ambaye ni mwimbaji mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyechanganya na ‘Uswideni’, Mohombi aliyeshiriki pia kwenye albam hiyo.

Mohombi ameshirikishwa kwenye wimbo namba 13 kwenye The Money Mondays unaoitwa ‘Kwangu Njoo’. Kwa mujibu wa Vanessa Mdee, ilimchukua saa 24 tu kutafuta na kukamilisha kolabo hiyo na kutumiwa sauti ya mkali hiyo.

 

Video: Vanessa aanika alivyovuta ‘Pumzi ya Mwisho’ kwenye misukosuko
Dk Shika aiaga bongo