Vikosi vya ulinzi na usalama vya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi na Magereza vimeungana kufanya mazoezi leo mjini Dodoma kwa lengo la kuwa tayari zaidi kudhibiti uhalifu.
Akizungumza wakati wa mazoezi hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema kuwa mazoezi hayo ya pamoja ni hatua ya kujiweka sawa kukabiliana na uhalifu wa aina yoyote na wakati wowote.
Kamanda Muroto ametahadharisha kuwa mtu yoyote atakayejitokeza kutaka kuharibu amani ya nchi atadhibitiwa kwa mujibu wa sheria.
Naye Kaimu Kamanda wa kikosi cha JWTZ, Ihumwa, Kanali Mtukusya amesema kuwa mazoezi hayo ni endelevu na kwamba ushirikiano huo utasaidia kuthibiti vitendo vya uhalifu.
“Hauwezi ukafanikisha kufanya kazi yako kwenye kitengo chako bila kuwa na mahusiano na chombo kingine. Nina imani kwamba haya mazoezi haitakuwa mwisho, tutaongea na makamanda wenzangu hapa ili tuone ni kitu gani kingine tunaweza kufanya kuendeleza ushirikiano kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama,” alisema Kanali Mtukusya.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo, Dkt. Bilinith Mahenge amesema kuwa hatua hiyo itasaidia upatikanaji wa taarifa za uhalifu kwa haraka kwa kuwashirikisha wananchi.
“Kwa sababu kama ataonekana mhalifu ambaye aliyetakiwa kumkamata ni polisi lakini uliyemuona ni wewe afisa magereza basi hakikisha unatoa taarifa kwa anayehusika ili aweze kushughulikiwa mara moja,” alisema.