Mshambuliaji wa Kimataifa kutoka DR Congo, Junior Kabananga amesema mpaka sasa hajapokea tuzo ya kiatu cha dhahabu, baada ya kuibuka kinara wa ufungaji bora wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2017).
Kabananga ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya Qatar SC ya Qatar, alifunga mabao matatu katika fainali hizo zilizofanyika nchini Gabon, na timu ya taifa ya Cameroon ilitawazwa kuwa mabingwa.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31, amesema mpaka sasa hajapokea tuzo hiyo, na amewahi kuwakumbusha viongozi wa shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kupitia shirikisho la soka nchini kwao (FECOFA).
Katika fainali za AFCON 2017, Kabananga aliiongoza timu yake hadi kufika robo fainali wakipoteza mbele ya Ghana. Magoli yake matatu yote alifunga katika hatua ya makundi dhidi ya Togo, Ivory Coast na Morocco.
“Sikuipokea tuzo yangu ya ufungaji bora kutoka (CAF) tayari nimewasilisha ombi langu FECOFA (Shirikisho la Soka DR Congo) hadi leo bado nasubiri nataka kuwa na tuzo yangu nyumbani katika nyumba yangu, sebuleni”.
Katika fainali hizo Cameroon walitwaa ubingwa kwa kuifunga Misri mabao mawili kwa moja.