Siku ya jana Nchi za Afrika mashariki zilisomewa makadirio ya bajeti kuu ya mapato na matumizi kwa kila nchi huku nchini Kenya kabla ya kusomwa vurugu ziliibuka baada ya wabunge wanawake kususia kikao cha mchana ambacho bajeti inasomwa.
Wabunge hao walisusia kikao cha kusomwa kwa makadirio ya bajeti ya nchi yao kwa kulalamikia hatua ya mwenzao kudaiwa kushambuliwa katika majengo ya Bunge na mbunge wa kiume.
Wabunge hao walitaka mbunge wa Wajir Mashariki, Rashid Amin kukamatwa kwa kosa la kumpiga mbunge mwakilishi wa wanawake wa jimbo la Wajir Fatuma Gedi, tukio ambalo lilijiri wakati bunge liliporejea kwenye kikao cha mchana cha usomaji wa bajeti kuu.
Wabunge hao walianza kuimba nyimbo za kumtaka mbunge Rashid ajiuzulu, pamoja na kiongozi wa wengi bungeni, Aden Duale pia ajiuzulu kwa kushindwa kutetea viongozi wanawake bungeni.
Kutokana na vurugu hizo, Spika wa bunge la Kenya, Justin Muturi alilazimika kuwaita maafisa wa ulinzi wa bunge ili kuwatoa nje wabunge waliokuwa wakizua vurugu muda mfupi kabla ya kusomwa kwa makadirio ya bajeti ya mwaka 2019/2020.
Lakini viongozi hao waliokuwa na hasira waliendelea kupiga mayowe wakisema “Hatutanyanyaswa na wanaume, tumechoka”, hadi pale agizo la spika lilipotekelezwa.
Imeripotiwa kuwa Rashid alimshambulia mbunge Fatuma katika eneo la kuegesha magari baada ya wao kutofautiana vikali kabla ya kumpiga makofi mbele ya walinzi.
Vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti kuwa Rashid alitaka kujua kwanini Fatuma ambaye ni mwanachama wa kamati ya bajeti, hakulitengea mgao wa fedha eneo la Wajir Mashariki wakati kamati ya bajeti ilipozuru eneo hilo hivi karibuni.
Vurugu hizo katika viwanja vya bunge la Kenya zilichukua takribani nusu saa na baadae wabunge hao wakarejea bungeni na Radhid Khasim kupelekwa kituo cha polisi.
Katika picha iliyosambazwa imemuonesha mbunge Fatuma akitokwa na machozi pamoja na matone ya damu mdomoni, kisa kilichozua pia mjadala mkali katika mitandao ya kijamii nchini kenya huku wengi wakionesha ghadhabu juu ya Mbunge Rashid kwa kutumia maneno #JusticeForFatumaGedi.