Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuziomba taasisi za fedha za kimataifa pamoja na nchi za Jumuiya ya madola kufikiria kufuta kabisa madeni yaliyokopeshwa kwa nchi zinazoendelea ili fedha hizo ziweze kutumika kupambana na athari zilizotokana na Covid 19.
Ombi hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamamba John Kabudi alipokuwa akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika mkutano wa Marais, Mawaziri Wakuu pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi na Serikali za Jumuiya ya Madola uliofanyika kwa njia ya mtandao (video conference) jana katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Prof. Kabudi amesema kuwa Tanzania imesisitiza tena umuhimu wa mashirika ya fedha ya Kimataifa pamoja na nchi za Jumuiya ya Madola zilizoikopesha Tanzania mbali na kutoa msamaha wa madeni waweze kufikiria kufuta kabisa madeni hayo ili kuziwezesha nchi zinazoendelea kuwa na fedha za kuboresha mifumo ya afya, pamoja na kupambana na athari zilizotokana na janga la covid 19.
Katika mkutano huo, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi za Jumuiya ya Madola na nchi zinazoendelea ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na umoja na mshikamano katika kupambana na janga la Covid 19.
“Mkutano huu umekuwa ni mkutano muhimu sana katika jumuiya yetu ya madola na tumesisitiza kuwa kuna umuhimu wa kushirikiana na kuwa na misaada na mipango madhubuti ya mashirika ya kimataifa kuzisaidia nchi zinazoendelea katika jitihada zake za kuboresha na kujenga viwanda vyake hasa vya kutengeneza dawa na vifaa tiba ili inapotokea majanga kama haya ya covid 19 ziweze kuwa na dawa na vifaa tiba kwa wananchi wake” Amesema Prof. Kabudi
Ameongeza kuwa, nchi nyingi mara baada ya janga la covid 19 zilizuia utoaji wa dawa na vifaa tiba kwenda nje ya nchi kwa sababu dawa hizo walizihitaji kwa ajili ya matumizi yao wenyewe ndani ya nchi, na ndiyo maana nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi Kusini mwa Afrika (Sadc) tumeiomba India kwa upendeleo kutupatia dawa na vifaa tiba vya kukabiliana na janga la Corona.
Aidha, mkutano umejadili pia umuhimu wa teknolojia katika kupambana na Covid 19 na kuboresha mifumo ya afya na kwamba wakati umefika sasa teknolojia hiyo mahali popote ilipo ndani ya Jumiya ya Madola iweze kutolewa kwa nchi zote kwa gharama nafuu ili kuziwezesha nchi mbalimbali kutumia mifumo mipya ya kiteknolojia katika mifumo yake ya afya na kuziwezesha pia kupambana na Covid 19.
“Ni vizuri tuwe na mipango madhubuti na mikakati ya kupambana na aina hii ya majanga ambayo yanaweza kujitokeza siku za usoni na kufanya hivyo ni kuanza kujiandaa sasa kwa kuimaraisha huduma za afya katika nchi zetu,” Amesema Prof. Kabudi.
Waziri Kabudi ameongeza kuwa Tanzania imeanza jitihada hizo kwa kujenga hospitali nyingi za wilaya, mikoa pamoja na vituo mbalimbali vya afya na zahanati.
Mkutano huo umejadili, masuala mbalimbali ikiwemo, covid19, biashara, uchumi, viwanda, uwekezaji pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.
Ikumbukwe kuwa Mwezi April, 2020 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliiomba Benki ya Dunia pamoja na mashirika ya fedha ya kimataifa kuzisamehe madeni nchi zinazoendelea ili nchi hizo ziweze kutumia fedha hizo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu Corona.