Baada ya kuteuliwa kuwa mịumbe wa Bodi ya Baraza la Ushauri Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameahidi kuhakikisha lengo mama la kuisaidia klabu hiyo kwa kila eneo linatimia na kuipa mafanikio zaidi.
Kaburu ni miongoni ya wajumbe 20 walioteuliwa na Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’ chini ya mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Thomas Mihayo.
Kaburu amesema kwake ni faraja kubwa kuteuliwa kuwa miongoni mwa washauri kwani inaonesha ni jinsi gani wadau wamekuwa na imani naye hata baada ya kumaliza kuwahi kuiongoza klabu hiyo.
“Ni imani kubwa iliyooneshwa kwangu kwamba nilishawahi kuwa kiongozi na sasa nimepewa nafasi ya kutoa mawazo yangu kwa uongozi uliopo,” amesema Kaburu aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Simba SC na kuongeza:
“Lengo kubwa ni lengo mama la kuhakikisha Simba SC inazidi kwenda mbali na inafikia malengo madogo na makubwa, kikubwa Simba SC ni Nguvu Moja hivyo mashabiki, wanachama wote tuwe pamoja na wawekezaji, wadhamini na uongozi kuhakikisha Simba yetu inafikia pale tunapotarajia.”
Mbali na Kaburu, wajumbe wengine ni Hassan Dalali, Ismail Rage, Evans Aveva, Faroukh Baghoza, Swedi Nkwabi, Azim Dewji, Kassim Dewji, Musley A-Ruweh, Mohamed Nassor, Mulamu Ng’ambi, Octavian Mshiu na Mohamed Janabi.
Wengineni Hassan Kipusi, Gerald Yambi, Moses Kaluwa, Crescentius Magori, Juma Pinto, Mwina Kaduguda na Idd Kajuna.