Mlinda Lango chaguo la tatu kwenye kikosi cha Young Africans Ramadhan Kabwili huenda akatemwa wakati wa Dirisha Dogo ambalo rasmi litafunguliwa Desemba 15.
Kabwili anatajwa kutemwa kwenye kikosi cha klabu hiyo Kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, sambamba na wachezaji wengine watatu ambao tetesi zinaeleza kuwa, tayari orodha yao imeshakabidhiwa kwa viongozi.
Hata hivyo hadi sasa Uongozi wa Young Africans umeendelea kuwa kimya kuhusu suala hilo, huku ukisisitiza muda utakapowadia kila kitu kitawekwa sawa.
Mpango wa kuachwa kwa Kabwili, unachagizwa na hitaji la Mlanda Lango mwingine ndani ya kikosi cha Young Africans inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa, kufuatia Chaguo la Kwanza Djigui Diara kutarajia kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Mali kitakachoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazounguruma mapema mwaka 2022.
Wachezaji wengine wanaotajwa huenda wakaungana na Ramadhan Kabwili ni Mabeki Adeyun Salehe na Paul Godfrey ‘Boxer’ pamoja na Ditram Nchimbi ‘Duma’ ambaye tayari inasemekana ameshasaini mkataba na klabu ya Geita gold FC.