Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Jeff Sessions amesema kuwa maafisa wa upelelezi wa serikali ya Marekani (FBI) wamemkamata mtu mmoja anayeitwa Cesar Sayoc, 56, anayeishi mji wa Aventura, Jimbo la Florida, FBI anayeshukiwa kuhusika katika tukio la kutuma vifurushi 12 vilivyo na vifaa vyenye uwezo wa kulipuka.
Vifurushi vingine viwili vilivyokuwa vimetumwa kwa seneta wa chama cha Demokratic, Cory Booker na aliyekuwa mkurugenzi wa idara ya ujasusi ya kitaifa, James Clapper vilikamatwa.
Maafisa wa FBI wamesema kuwa vifurushi hivyo vinavyo fanana na mabomu yaliyotumwa kwa maafisa wengine wa ngazi ya juu, nchini Marekani, vilikamatwa katika jimbo la Florida kabla ya kuwafikia walengwa.
Aidha, wengine waliolengwa katika tukio la kutumwa mabomu ni Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama, na waziri wa mambo ya nje wa zamani, Hillary Clinton, maafisa wengine wa chama cha Democratic, wakosoaji wa Rais Donald Trump na shirika la habari la CNN.
Hata hivyo, Rais wa Marekani, Donald Trump amevilaumu vyombo vya habari vya nchi hiyo kwa kuongeza hali ya chuki za kisiasa nchini Marekani, ambayo wachambuzi wamesema imeleta uhasama na majaribio kufanya mauaji.