Mahakama nchini Australia imemtia hatiani Kadinali, George Pell wa Kanisa Katolili kwa kosa la kuwanyanyasa kingono na kuwabaka wavulana wawili.
Jopo la majaji limefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa Kadinali Pell aliwaingilia wavulana wawili, mmoja akiwa na umri wa miaka 16 waliokuwa waimba kwaya, katika nyumba moja ya Kanisa mwaka 1996. Hata hivyo, alikana kutenda makosa hayo.
Kwa mujibu wa CNN, uamuzi wa Mahakama ulifikiwa Desemba mwaka jana lakini haukutangazwa kutokana na taratibu za kisheria, ambapo leo umewekwa wazi mahakamani.
Pell mwenye umri wa miaka 77 ambaye alikuwa na cheo cha uweka hazina wa Vatican, alikuwa mmoja kati ya viongozi wenye nguvu katika kanisa hilo. Amekuwa mtumishi mwenye cheo kikubwa zaidi katika kanisa Katoliki kuwahi kupatikana na hatia ya kosa la unyanyasaji wa kingono na ubakaji.
Kesi yake ilisikilizwa mara mbili, baada ya mara ya kwanza jopo la majaji kushindwa kufikia uamuzi kutokana na kutotimia kwa akidi. Jopo la pili lililokuwa na majaji watatu lilikamilisha kesi hiyo kwa maamuzi ya kumtia hatiani.
Hukumu dhidi yake inatarajiwa kutolewa hapo baadaye, lakini yeye amedai kuwa atakata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.
Hivi karibuni, Papa Francis ambaye ndiye Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki alikiri kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kanisa ikiwa ni pamoja na mapadri na maaskofu wanaowanyanyasa kingono ‘masista’, watoto wadogo na hata waumini wengine.
Alitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya watumishi wanaoripotiwa kuhusu vitendo hivyo. Alisema kuwa vitendo hivyo ni aibu kwa Kanisa na dunia kwa ujumla na kwamba havivumiliki hata kidogo.