Katika kuhakikisha timu ya taifa ya Tanzania ya soka la Ufukweni inakuwa na nguvu zaidi kuelekea Faini za Afrika za Soka la Ufukweni (BSAFCON2021),  Kocha mkuu wa timu hiyo Boniface Pawasa amemuongeza kikosini kipa wa Mtibwa Sugar, Shaban Kado.

Pawasa amemuongeza mlinda mlango huyo mkongwe kikosini kwake, kwa lengo la kuongeza chachu ya ushindani kwa walinda milango wengine ambao waliwaita siku kadhaa zilizopita.

Kocha huyo amesema anahitaji kuwa na kikosi imara kuanzia nafasi ya mlindamlango hadi ushambuliaji, hivyo ameonea uwepo wa Kado kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Soka la Ufukweni, kutaleta tija kubwa.

“Tulikuwa na makipa wawili na mpango wa kumuongeza Aron Karambo wa Dodoma Jiji lakini ratiba yake ilimbana na kushindwa kujiunga nasi ndipo pendekezo jingine likawa Kado.

“Kumbuka tunaenda kwenye michuano ya Kimataifa hivyo tunatakiwa kuwa na makipa watatu bora na wenye uzoefu, tunaamini atatusaidia.” amesema Pawasa.

Tanzania ilifuzu Fainali za Afrika za Soka la Ufukweni baada ya kuifunga Burundi katika michezo ya kuwania kufuzu, iliyochezwa jijini Dar es salaam mapema mwaka huu.

Katika Fainali za Afrika za Soka la Ufukweni zitakazounguruma nchini Senegal kuanzia 23–29 Mei 2021 , Tanzania imepangwa kundi A na timu za DR Congo, Uganda pamoja na wenyeji Senegal.

Itaanza kucheza dhidi ya Uganda Mei 24, mchezo wa pili Tanzania itapambana dhidi ya DR Congo Mei 24, na mchezo wa mwisho wenyeji watamaliza dhidi ya kikosi cha Pawasa Mei 26.

Rais Samia abadilisha Wakuu wa Mikoa wawili
Waziri Bashungwa awaita mashabiki kwa Mkapa.